UTANGULIZI:
Ndugu yangu kuna shuhuda nyingi sana zinazoanguka duniani, lakini wachache wanaozingatia kwa vile watoaji si wa dini zao au si wa madhehebu yao wala hawajulikani makanisani. Sasa ninakuomba ewe msomaji, tafuta mahali pa utulivu, mwombe Mungu na kusoma ushuhuda huu ili upokee kile ambacho Bwana amekuletea leo.
Msichana Nyisaki Chaula alionyeshwa na Bwana ushuhuda huu akiwa na umri wa miaka 16 mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Ushuhuda huu alionyeshwa akiwa ameokoka na si kwamba alikufa bali aliona maono. Maono haya alionyeshwa kati ya tarehe 30 – 31/12/1991; yaani kwa siku mbili tofauti.
Msichana huyu hivi sasa ameolewa na Mwinjilistii Lemsy Mheni pale Uyole Mbeya kwa lengo la kukuza huduma yao. Kabila lake ni Mkinga wa Makete, Msichana huyu anapatikana Uyole njia panda ya Malawi – Zambia na Dar es Salaam pembeni mwa kituo cha mafuta ya magari pale Uyole, Bwana awatangulie katika usomaji.
SURA YA 1
KUITWA:
Ilikuwa ni mwezi wa 12/1991 tulipochaguliwa vijana 10 kuombea Mkutano wa Kiroho ambao ulikuwa ukifanyika pale Uyole. Siku moja baada ya maombi ya usiku, nilala pamoja na dada zangu. Siku hiyo nilala usingizi mzito ambao sijapata kuona. Usiku nilishangaa kukuta usingizi umetoweka kabisa, hivyo nikabaki nikiwa macho, ndipo nikasikia sauti ikiita ‘Nyisaki’ nikasikia lakini sikuitikia, ikaita mara ya pili pia sikuitika. Hata mara ya tatu ndipo nikaitika kisha nikasikia ile sauti ikisema ‘Nimekuchagua kuwa mtumishi wangu’ ndipo nikatambua kuwa ni sauti ya Bwana, nikasema “Bwana mimi ni motto mdogo tena hata chuo chochote sijaenda nitawezaje kuifanya kazi hiyo? Bwana akaniambia mkumbuke Yeremia mtumishi wangu nilimchagua angali bado mdogo (Yeremia 1:5) basi nikaendelea kubishana na ile sauti hadi dada yangu mmoja aliamba na kusema ‘Mshukuru Mungu kwa sababu amekuchagua wewe’.
Ndugu msomaji kumbuka kuwa sauti hiyo nilisikia nikiwa macho kabisa na wala haikuwa ndoto na baada ya kusikia sauti hiyo mara ya pili na ya kwanza niliamka na kuthibitisha kabisa kuwa wote niliokuwa nimelala nao bado wamelala. Na hata huyo dada yangu alisema ‘Mshukuru Mungu kwa sababu amekuchagua wewe’ nilitambua kuwa ni Mungu ndiye aliyemuelimisha na kumfunulia jambo hili.
Baada ya yote haya tukamshukuru Mungu na kulala. Kesho yake tarehe 30/12/1991 ndipo nilipoonyeshwa mambo makuu ya ajabu (Yeremia 33:3)
SURA YA 2
JEHANAMU SEHEMU YA KWANZA NA MANGOJEO YA WAFU:
Ikiwa tarehe 30/12/1191 tulipoamka tukaenda kwenye semina na baada ya ile semina tuliamua kwenda kumuona rafiki yetu aliyeokoka ambaye kwa muda ule alikuwa hajiwezi yaani alikuwa anaumwa. Tulipofika pale nyumbani tukafungua ibada kwa maombi kisha tukaanza kujifunza jinsi Biblia inavyosema kwa njia ya maswali. Hata baada ya hapo tukaamua kufunga Ibada kwa maombi kama tukivyofungua.
‘Tufunge kwa maombi na kumkabidhi ndugu yetu mikononi mwa Bwana, maana tulianza ibada yetu kwa kumshukuru Mungu kwa kuwa ndugu yetu alikuwa hajambo’ Ninachokumbuka ni kwamba tuliimba pambio moja ya kuabudu lakini sikumbuki kwamba tuliingia kwenye maombi au la tulipokuwa tunaimba ile pambio ya kuabudu, nikashangaa kuona kuwa nimechukuliwa niko sehemu tofauti kabisa na mazingira ya nyumbani.
Ukiniuliza kuwa nilichukuliwa vipi hata mimi mwenyewe sielewi, lakini nilishangaa kuona kwamba niko kwenye bonde moja kubwa sana, na lile bonde lilikuwa halina miti wala majani wala ndege na vitu vilivyopo duniani, sehemu yenyewe ilikuwa haivutii hata kidogo, ni sehemu moja iliyokuwa na ukimya wa aina yake. Sasa nikashangaa mbona nilikuwa na rafiki zangu na sasa siwaoni, nikaendelea kujiuliza ni nani aliyenileta huku, na hapa ni wapi? Basi niliamua moyoni mwangu kuwa liwalo na liwe kwa sababu sijui hata aliyenileta mahali hapa, nilikuwa nimekata tamaa, nikajiandaa kutaka kukaa ndipo nikasikia sauti nyumba yangu ikisema ‘Nyisaki nifuate’. Nilipoinuka nilishangaa sana kumuona mtu mmoja mfano wa mwanadamu nilipomtazama yule mtu, umbo lake hakuwa mrefu sana wala hakuwa mnene sana, alikuwa ni mtu ambaye sijawahi kumuona popote duniani. Nywele zake zilikuwa ndefu na alikuwa amezibana nyuma kwa banio jekundu, alikuwa amevaa vazi refu mpaka miguuni na jeupe sana ambalo hata weupe wake sijawahi kuuona hapa duniani. Alikuwa ni mweupe sana, siyo weupe wa hapa duniani, macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, huyo mtu alikuwa hakanyagi chini bali alikuwa akitembea hewani na vazi lile lilikuwa liking’aa sana haliwezi kabisa kutazamika kwa macho ya binadamu. Nayasema mambo ambayo niliagizwa niyaseme, huyu mtu alikuwa amejifunga mkanda mmoja mwekundu kiunoni ndipo nikaamka nikaanza kumtuata. Baada ya hatua chache nikaanza kusikia muungurumo Fulani ambao ulinitisha kwa kiasi Fulani lakini sikuuliza. Kadiri tulivyozidi kutembea mbele ndivyo muungurumo ulivyozidi kuongezeka na kutisha zaidi, mara nikasikia sauti yangu ikiniambia inua macho na tazama mbele, ndipo nikashituka sana nilipoona moshi mkubwa mnene na mweusi umefunika bonde lile na kusababisha giza nene katika bonde. Nikamuuliza yule mtu huko mbele kuna nini? Yule mtu akasema, ‘hiyo ni Sehemu ya Jehanamu watakakoenda watenda dhambi baada ya maisha ya duniani’ Baada ya kusikia hayo yote ndiyo nguvu zikaniishia, nikaanza kulia na kumuomba sana Mungu anisamehe maana kwa mawazo yangu nilifikiri nimekufa na sasa napelekwa Jehanamu nikaendelea kulia sana hadi yule mtu aliponieleza usilie maana ukilia utashindwa kuwafikishia watu wangu habari hizi. Hofu ilijia nilitishika mno, lakini mpango wa Mungu kunionyesha mambo haya ni kuwaambia watu.
Ndugu msomaji, kweli Jehanamu ninavyoelezwa kuwa ni ziwa la moto elewa hivyo. Nilipotazama sikuona mwisho wake, bali niliona milipuko mikubwa sana na ya kutisha na milipuko hiyo haikufanana na milipuko yoyote hapo duniani labda kwa sehemu inayoweza kulinganishwa na milipuko ya visima vya mafuta.
Milipuko hiyo ni mikubwa na inatisha mno iliyosababisha moshi mkubwa sana ulioambatana na moto wa kupaa juu. Moto ule ulijichanganya changanya kama vile bahari iliyochafuka. Kulikuwa na mawimbi makubwa na ya kutisha na yakichanganyika na kutoa miungurumo mikubwa ambayo haiwezi kumfanya mwanadamu kusikia hata mateso ya mwenzake. Mimi nilipokuwa nasikia habari ya Jehanamu nilifikiri labda ni moto mdogo au makaa ya moto. Lakini siku hiyo niliyoona mwenyewe kiasi kwamba nilibaki kulia na kuomboleza kwa uchungu mkubwa mno. Mtu yule alifanya kazi ya kunionya nisillie, pia alinitia nguvu na ndipo nilipoweza kuendelea, ndugu yangu ukisikia Jehanamu iogope kama ulivyo.
Nilipoangalia ndani ya ule moto niliona vitu vyenye uhai virefu vyeupe nikauliza hivyo ni vitu gani? Yule mtu akasema ‘hao ni funza wa Jehanamu’ hizo rangi kwenye pingili zake ni za nini? Akasema hivyo siyo rangi, kama unavyowaona hao funza wana meno hayo manne yenye uwezo hata wa kutoboa fuvu la kichwa cha mtu, na huyo funza akishaingia ndani huacha sumu kali (yahani hiyo unayoiona kama rangi ambayo humtesa mwanadamu milele na milele.
Hao funza walikuwa ni wengi sana lakini hawafi ndani ya ule moto, (Marko 9:45-46) walikuwa wembamba warefu yapata mita moja, na walikuwa na pingiri pingiri ambazo zilionekana kuwa na rangi, walikuwa na meno mawili mbele na kichwani kulikuwa na meno mawili jumla ya meno yote manne, yaani mkiani na kichwani kulikuwa na midomo.
Bwana akasema ‘ hawafi wala hawaugui kwa sababu wamehifadhiwa kwa ajili ya mateso ya watenda maovu’
Ndugu msomaji, nisingeweza kupoteza muda wangu kukuletea jambo ambalo sijaliona lakini nimesema haya ili ukiwa na masikio na uyasikie, ukikataa ni juu yako mwenyewe. Maana sikuambiwa kwamba nimlazimishe mtu aokoke, bali niliambiwa nikamwambie kila mtu labda atakuwepo mmoja atakayegeuka na kuponywa. Sasa nikauliza mbona watu wanasema Jehanamu kuna wanaoungua lakini iweje Jehanamu hii haina watu wanaungua? Akasema wanasema kweli lakini watu watakuja kutupwa kwa wakati wake. Lakini muda huu wamehifadhiwa wakimsubiri baba yao aliyewadanganya (yaani shetani).
Akasema twende nikakuonyeshe nikaanza kumfuata. Kweli ndugu zangu Jehanamu uisikie kama ilivyo. Nilipofikiri habari za wale funza wa ajabu kwa kweli nililia kwa uchungu mkubwa mno nilitetemeka na kuishiwa nguvu nikaanza kuwaza moyoni mwangu mtu anayejua dhambi ni mbaya, na anajua neema ya Mungu na kupuuzia kweli uje kuteswa katika ziwa hili la kutisha lenye moto usiozimika na funza ambao hawafi, kwa kweli nililia sana. Lakini yule mtu akaniambai nyamaza, maana ukilia utashindwa kuyafikisha yote ninayotaka kukuonyesha. Kwa kweli nashindwa hata nieleze vipi. Jehanamu ni kweli ipo na inatisha sana; achana na mafundisho ya mashetani yanayosema hakuna Jehanamu na ukiendelea kufuata hayo utaangamia na kujuta milele. Ninaeleza ndugu yangu kuwa Mungu hapendi upotee ndiyo maana amekupa nafasi kama hii. Nayo yawezekana ni nafasi ya mwisho sasa usipokubali kutubu yawezekana ukajiletea maangamizi wewe mwenyewe.
JEHANAMU IMEANDALIWA KWA AJILI YA SHETANI NA MALAIKA ZAKE:
Niliondoka sehemu hii ya Jehanamu na kuelekea sehemu ya mangojeo nikiwa nalia kwa uchungu mkubwa mno. Na haya ninayokuambia sikutishi bali nakuambia kweli na kama unafikiri nakutisha basi utakwenda kuona mwenyewe.
Nikaenda kumfuata yule mtu, tulipofika mahali fulani na kutazama bondeni niliona bonde kubwa lililokuwa limefunikwa giza la kutisha mno. Kabla ya kuwafikia wale
watu nilisikia sauti za watu zikilia kwa uchungu mkubwa mno, ndugu yangu kweli Jehanamu kuna vilio vya aina yake, vilio ambavyo huwezi kulia kama walivyokuwa wakilia wale watu, wanalia bila kupumzika. Lile giza nene mno linawafanya wale watu wasiwaze kutazamana kila mmoja na kilio chake na kila mtu na mateso yake hakuna mtu ayakayeondoka kwenda kumfariji rafiki yake, kwa sababu kila mmoja aliomboleza kwa ajili ya mateso yake, kadiri tulivyozidi kuteremka lile bonde ndivyo lile giza lilivyozidi kutoweka.
Ndipo tulipofika kule bondeni niliona watu wengi mno wasio na idadi; ni wengi kama weusi wa duniani, hakuna mzungu wala mwafrika wote ni weusi kupita kawaida. Na weusi uliosababishwa na baridi kali sana inayopatikana sehemu ile. Na ndimi zao zilikuwa zimevutwa hadi kufikia kila mtu kifuani pake, awe mrefu au mfupi. Nikauliza mbona ndimi zao watu hawa zinafika kifuani? Yule mtu akasema unavyoona sehemu hii haina maji wala haina furaha yoyote, sasa hizo ndimi wanazitumia kwa kulamba machozi, machozi haya hupatikana kwa kilio cha miezi mingi sana kupita na ndipo inatokea chozi moja ambalo hulitumia kama maji. Ndipo nikashikwa na uchungu wa ajabu nikakumbuka hawa ni watu walioishi chini ya Neema ya Mungu, lakini baada ya kufa kwao wako sehemu ya Jehanamu wakimsubiri baba yao aliyewadanganya. Kulikuwa na wanawake na wanaume.
Watu wale walikuwa wakilia kwa uchungu mkubwa mno. Nikamwomba yule mtu, nikisema Bwana naomba wachukue watu 100 kutoka kila nchi ili waone hii Jehanamu wawaambie wanadamu watageuka. Akasema wanadamu ni wenye mioyo migumu hata angerudi Yesu mwenyewe wasingemwamini wangeendelea na dhambi. Basi nikaendelea kulia sana. Kisha akaniuliza kama nilikuwa nawafahamu wale watu, nikasema siwafahamu. Akasema twende huku, nikaendelea kukatiza katikati ya mabilioni ya watu waliofia dhambi, kila mmoja na uchungu wake na kila mmoja na mateso yake.
Hata wa kwanza kumuona alikuwa Babu yangu mzaa Mama, yeye alikuwa ni Mwinjilisti na Mzee wa Kanisa katika kanisa la Lutherani kule Isapulamo Makete, sasa nilishangaa sana kumuona katika sehemu hii ya Jehanamu, yeye akiwa duniani alikuwa mweupe sana. Lakini sasa nilishangaa kumuona akiwa mweusi kupita kawaida. Nikamuuliza mbona mtu huyu alikuwa mtumishi wa Mungu na sasa namuona sehemu hii? Yule mtu akasema kweli kabisa huyu mtu alichaguliwa kwa ajili ya kazi ya Mungu lakini aliamua kuifanya kazi ya Mungu na kuingiza michanganyo. Na ndiyo maana ukamuona sehemu hii, ulevi kidogo alikuwa nao, ushurikina kidogo na mambo mengine kama hayo, kama maandiko yasemavyo Ufalme wa Mungu wanauteka wenye nguvu tu. (Matayo 11:12)
Mtu wa pili alikuwa jirani yetu, alikuwa ni kaka mmoja aliyekuwa anasali kanisa la Moraviani. Alikuwa ni kaka mmoja aliyejipenda sana na kila siku ya ibada na Jumapili alishika Biblia na kitabu cha nyimbo, kumbe alikuwa hafanyi mapenzi ya Mungu. Hata leo ukienda Uyole utasikia sifa zake. Huyu kaka alikuwa anaumwa sana na amelazwa katika hospital ya Mbeya, siku mbili kabla ya kufa kwake alituma watu kwenda kumuita mchungaji amwombee na baada ya siku mbili akafa. Sasa nikashangaa sana kumuona sehemu hii ya mateso, wakati huo huo wanasema mtu akiombewa anakwenda moja kwa moja mbinguni? Yule mtu akaniambia kawaambie watu wote duniani, mtu yeyote aliyejua kuwa dhambi ni mbaya na atakwenda Jehanamu, akisema nitatubu, nitatubu nikiona kwamba nimekaribia kufa, mimi huyo simpokei. Jinsi ninyi msivyopokea vitu vilivyooza ndivyo na mimi sivipokei japokuwa navitoa duniani (Ufunuo 22) Yule kaka akasema ninakuomba kawambie mama, baba na ndugu wasitende dhambi japokuwa mimi nimepata bahati mbaya kuja sehemu hii lakini kawaambie wasitende dhambi. Yule mtu aliyekuwa ananiongoza akasema usiende kuwaambia kwasababu duniani kuna wachungaji na waliookoka wanahubiri Injili wasipowasikia hao, nyumba nzima watakuja huku (Luka 16). Yule kaka akajitupa chini akalia kwa uchungu mkubwa mno.
Mtu wa tatu kunionyesha alikuwa Mama yangu mdogo upande wa Mume wangu (Alipokuwa anasafiri mme wake) akakorofishana na wakwe zake ( yaani wazazi wa mume wake) basi akanywa vidonge akafa, mume wake aliporudi na kuonyeswa kaburi mkewe akachukua vidonge akanywa sasa tulipokuwa tunaenda kwa rafiki yetu kumuona ndipo tulipishana na gari iliyokuwa inampeleka hospitali akiwa mahututi. Sasa nikashangaa sana kumuona katika ile sehemu ya mangojeo. Nikauliza huyu mtu niliyemwacha duniani na sasa namuona huku? Yule mtu akasema, kawaambie ndugu zake duniani, mtu anapokufa duniani ile sekunde moja tu, huku amekuwa ameshiriki kiasi cha kutosha, kama ni mtu wa uzima amekuwa na uzima na amekuwa mwenyeji, sasa huyu mtu hapa unavyomwona hata dakika kumi na tano hajamaliza. Nilishangaa sana maana alikuwa mweusi sana, ulimi wake umevutwa na kufika kifuani kama wale wengine. Alionekana kama mtu aliyekaa kwenye mateso yale zaidi ya miaka elfu kumi. Moyo wangu ulijaa huzuni na uchungu usio wa kawaida, basi yule mtu akaniambia sasa ‘kawaambie watu wote jinsi ulivyoona, na jinsi ulivyosikia usiongeze wala usipinguze atakayekataa usimlazimishe wala kumbembeleza, atakayekubari mwongoze sala ya Toba’.
Ndipo nikashangaa natokea katika nyumba ya yule rafiki yetu, wenzangu wote wametulia wakisubiri litakalotokea basi nikawaeleza yote niliyoyaona na kusikia basi tukamshukuru Mungu.
SURA YA 3
YERUSALEMU MPYA:
Siku ya tarehe 31/12/1991 niliongozwa na Mama kwenda shambani. Nilimweleza habari zote za baba yake, lakini mama hakuwa na la kufanya zaidi ya kusikitika, kwa maana nafasi ya baba yake ina gharama wala haina budi kuiacha hata milele (Zaburi 49:7-8)
Baada kufika shambani nilichimba shimo la kwanza, la pili na tatu kwa ajili ya kupanda mahindi, mara nikaanza kujisikia vibaya, basi nikamwambia mama akasema mwanangu hivi sasa ni saa tatu asubuhi watu wakikuona unarudi nyumbani watashangaa sana, vumilia kidogo. Sasa sikumbuki kama niliongeza kuchimba shimo au hapana. Nilishangaa niko kwenye sehemu nyingine ya tofauti kabisa na mazingira ya dunia, sehemu hii ilikuwa inaleta matumaini sana.
Sehemu hii ilinivutia mno basi nikawaza moyoni kama asipotokea yule mtu wa jana nitang’ang’ania huku huku. Nikaamua kukaa mara nikasikia sauti nyuma yangu ikisema ‘tufuate’ nilipogeuka nikashangaa kuwaona watu wawili waliofanana sana na mtu wa jana katika hali zote. Mmoja ameshika upanga na alisema anaitwa Mikaeli na aliyekuwa ameshika karatasi alisema alisema anaitwa Gabriel, Wasomaji wa Biblia wanajua kazi zao (Daniel 10:13, Yuda 1:9, Luka 1:26)
Nasikia sauti ndani yangu ikiniambia, inua macho yako utazame mbele nilishangaa sana kuona mbele yetu kulikuwa na nuru kubwa sana kutoka katika mji mmoja mkubwa na mzuri ajabu. Nuru ile iliangaza vizuri kuliko hata mwangaza wa jua na mwezi. Kwa kweli nilivutiwa sana na mji ule jinsi ulivyo na unapendeza. Nikauliza ule mji ni mji gani? Na ni kwa ajili ya nini? Wakaniambia ‘Ule ni mji Mtakatifu, Yerusalem mpya na ni kwa ajili ya Watakatifu walioshinda ya dunia’ Kwa kweli nashindwa hata kuelezea uzuri wa mji ule maana hauna mfano wa aina yoyote hapa duniani. Tumani langu ni kwenda kuishi katika mji wa utukufu mwingi sijui mwenzangu unatumaini gani?
Tulipofika mlango wa lile jiji, mawazo yangu yalinipeleka moja kwa moja katika tenzi namba 121 ‘’Liko lango moja wazi’’ Niliona lango moja kubwa lililokuwa wazi, (Ufunuo 3:7-8) lango hili lilikuwa likibadirika kila aina ya rangi, nyingine hazipo duniani. Tulipoingia ndani karibu na mlango tulimwona mtu mmoja mzuri sana mweupe na aling’aa sana, alikuwa amekalia kiti kizuri na cha thamani kupita kawaida. Alionekana kuwa mtu mpole mwenye huruma sana na upendo, (Mithali 11:28-30) tabasamu lake lilinipa raha ya aina yake na kuifanya nicheke sana kwa furaha na kujisahau. Malaika nilioongozana nao walianza kuzungumza na yule mtu kwa lugha nisiyoifahamu. Mimi nikaendelea kushangilia ule mji, ule mji umetengenezwa kwa vioo vitupu. Kila sehemu nilipotazama nilijiona mwenyewe (Ufunuo 21:18) nikaendelea kushangilia ule mji kwa uzuri wake na thamani yake hadi pale wale malaika waliponiambia tufuate.
Malaika walinitembeza mji mzima kwa muda mfupi sana hata sekunde moja haikuisha, nilishangaa sana sujui wametembea vipi wale watu. Malaika wa Kwanza akafungua mlango akaingia wa kwanza, pili nikaingia. Katika sehemu hii niliviona viti vingi sana vilivyokuwa vimeandikwa majina kwa damu mbichi. Vile viti vilikuwa vizuri na vya thamani kupita kawaida. Nikaomba kukalia kiti kimoja nikaambiwa utakalia ukishinda ya duniani.
Katika sehemu zote sikuona taa zikiangaza lakini kulikuwa na mwanga mzuri sana. Nikauliza mwanga huu unatokana na nini? Akaniambia mwanga huu ni wa mwanakondoo uliyemkuta mlangoni.
Nilipoingia kila mahali niliduwaa kwa kustaajabu ule uzuri wa mji ule. Kila mlango ulibadili baina ya rangi. Tukaondoka sehemu hii. Akafungua mlango mwingine nikastaajabu kuona bustani nzuri sana iliyozungukwa na maua ya majani yote yalikuwa na urefu sawa bila kuzidiana. Tena yalikuwa ya kijani kibichi sana. Maua ya sehemu hii marefu na yanamsifu Mungu kupita kawaida, yakiinama upande wa kulia yanakwenda yote na kusujudu na kuinuka hutoa harufu nzuri sana inayoenea mji mzima, maua hayo yalikuwa yamezungukwana kioo. Nikasema naomba nichume ua moja nikawaonyeshe ndugu zangu. Akasema maua ya huku hayachumwi, nikasema bustani hii imetengenezwa kwa hajili ya utukufu wa Mungu, nilitamani sana kukaa sehemu hii ya bustani, lakini wakasema tufuate.
Kila mahali tulipokwenda mmoja akafuata mwingine, nikasikia sauti nzuri mno zikiimba kwa furaha sana tukaingia, nikashangaa sana kuona watu wengi sana wasio na idadi. Nikajiuliza kwa nini Mungu anasumbuka kuwatafuta wanadamu wakati anao wengi sana? Nikastaajabu sana nikakumbuka pambio moja inayosema; Ukiringaringa kwa Yesu kuna watu wengi. Hawa watu walikuwa wanadamu kama sisi ambao waliishi duniani, lakini wao walimwishia Mungu na kufa na utakatifu.
Kama umewahi kuona mapacha basi wale ni mapacha wa aina yake. Sura zao hazitofautiani hata kidogo wamefanana sana hisivyo kawaida. Nywele zao zilikuwa ndefu wamezibana na banio jekundu sana, wala si wembamba sana na milifanikiwa kugundua tofauti moja tu. Wengine wamevaa mikanda miwili kiunoni na wengine mkanda mmoja. Nikauliza kuna tofauti gani kati ya waliovaa mkanda mmoja na waliovaa mikanda miwili? Akasema waliovaa mmoja ni wanaume na waliovaa miwili ni wanawake. Lakini ilikuwa sio rahisi kuwatofautisha kuwa huyu ametoka Taifa hili na yule Taifa lingine, waliimba wimbo mzuri isivyo kawaida, staili za uimbaji wao kwa kweli zilinifurahisha mno, walipunga mikono yao wote kwa pamoja na hapakuwepo hata mmoja wao aliyekosea. Nilipozidi kuwatazama nilitamani sana kujiunga nao ili nami niimbe na kumsifu kama wao wanavyosifu, lakini haikuwezekana kwa sababu hata lugha yao nilikuwa siijui. Baada ya muda akatokea dada mmoja na kuja upande wangu, niliweza kujua ni mwanamke kwa sababu alikuwa na mikanda miwili, nilishangaa kumuona yule dada kwa sababu niliweza kumtambua baada ya sura yake ile ya duniani kutokea. Yeye alikufa mwaka 1987 mwezi wa nne na aliuawa kwa kupigwa risasi. Yeye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari (Mbeya Day) kidato cha tatu (Form Three). Aliponifikia alisema ‘Ah Nyisaki, umekuha huku’ nikasema ‘Ndiyo’ akasema ‘Za duniani’ nikasema ‘Duniani matatizo’, akasema ‘Kweli matatizo. Angalia wenzenu tumevikwa miili mipya isiyoharibika, isiyopata magonjwa’ yaani aliusifu mwili wake na ni kweli ndivyo alivyo (1Korintho 15:40-53) akasema ‘Mwili wa zamani tumeuacha pale’, basi nikageuka niangalie amesema wapi, kweli ndugu yangu Biblia inasema mtafuteni Bwana maadamu anapatikana, mwiteni maadamu ya karibu (Isaya 55:6-7) mambo ya Uyole niliyaona kama vile unavyoweza kutazama kitu kwenye kiganja chako. Nilipoangalia sokoni nikaona biashara zinaendelea kama kawaida, barabarani magari na baiskeli ziliendelea kupishana kama kawaida, nilipotazama makaburini aliponionyesha huyu dada, nikaona makaburi ya watu wengi tena niliweza hata kusoma majina yao. Pia niliweza kujua wazi kabisa kuwa huyu yupo uzimani au jehanamu. Na kama hayupo ilionyesha wazi yuko uzimani. Kaburi la huyu dada lilionekana pia likiwa limepambwa maua. Akasema ‘umekiona kile kitu?’ Nikasema ndiyo, akasema ‘Ule ni mwili wako’. Kwa kweli sikupenda kuutazama mwili mara mbili, mwili wangu niliuona kama ngozi ya kenge chafu sana akaniambia geuka tena, nikakataa, mara ya pili nikakataa, mara ya tatu nikageuka nikaona kama mtu analima na kupanda mbegu akasema yule ni mama yako, fahamu zake tunazo huku, atarudishiwa fahamu utakaporudi wewe. Maono ya siku hiyo yalikuwa ya muda mrefu, kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni. Nilipochukuliwa kwenye maono mama alibeba mwili wangu kuweka kivulini, hapo ndipo nilitambua kweli fahamu zake zilichuliwa. Yule dada akasema Nyisaki kawaambie ndugu zangu wasitende dhambi tena katika mji huu hakuna huzuni, lakini ninawaona wanaendelea na dhambi nasikitika sana, wale Malaika wakasema ‘Usiende kuwaambia kule kuna walio’koka wanahubiri Injili, wasipowasikia hao basi ’
Mtu wa pili kunionyesha alikuwa mzee mmoja wa makamo aliyedharauliwa sana pale Uyole, alidharauliwa kwa sababu yeye alikuwa rafiki wa Biblia na Tenzi za Rohoni na kila alipojipumzisha iwe ni shambani, nyumbani au sehemu nyingine yoyote alisoma Biblia, aliimba Tenzi na kuomba, kweli yule alijishusha (Luka 14:35, 18:17, Isaya 51:7-8) watu walisema amechanganyikiwa. Nilishangaa kumuona katika sehemu hii akiwa kama kijana wa miaka ishirini (20), naye pia aliusifu mwili wake isivyo kawaida, kweli miili ile ni mizuri sana akasema kawaambie wapendwa wa duniani kila mmoja ajitahidi ashinde ya duniani maana muda umeisha, (Ufunuo 22:10-14) kila mmoja aangalie shetani asimpumbaze maana tuna hamu kubwa kuwaona wapendwa wetu, akaondoka akachanganyikana na wenzake.
Akatokea mtu wa tatu naye nilimtambua kuwa ni mwanaume kwa sababu ya ule mkanda mmoja, aliponikaribia ikatokea sura ya duniani, yeye alikuwa mzee wa Kipentekoste, alikuwa anasali Kanisa la Assemblies, akasema ‘Ah Chaula umekuja huku’ nikasema ‘Ndiyo’, ‘Za duniani?’ ‘Duniani matatizo’ akasema ‘Kweli matatizo, angalieni wenzenu tumevikwa miili mipya isiyosikia njaa, isiyopata magonjwa’ Basi aliusifu ule mwili, kweli alikuwa amebadirika naye alionekana kama kijana wa miaka ishirini (20) baada ya hapo akaondoka akaendelea kuimba. Baada ya kuonana na hao watu nikawauliza hao Malaika, hivi hawa watu wanajifunza kuimba? Wakasema kwa nini unasema hivyo, nikasema wanaimba wimbo hauishi akasema sivyo kama mnavyoimba duniani, maana duniani mkiimba dakika tano mnasema tumemsifu sana Mungu na wengine wanadhani wataenda mbinguni kwa sababu ya uimbaji bila kuokoka. Wimbo mmoja wa huku unaimbwa kwa miezi tisa, beti moja miezi mitatu, ‘’Chorus’’ miezi mitatu na beti ya mwisho miezi mitatu, basi nikashangaa sana. Tukaondoka hii sehemu akasema twende nikakuonyeshe watakatifu waliokuwako mwanzo wa kanisa, maana wameletwa sehemu yao akafungua mlango, tukaingia nikaonyeshwa watu kumi na sita (16), lakini nilijua wazi walikuwako na wengine zaidi
Mtu wa kwanza alikuwa Batholomayo, naye akanikumbatia na kunishika mkono, akasema Bwana ndiye aliyechunwa ngozi kwa sababu ya Injili. Na mtu wa pili kunionyesha alikuwa ni Yohana Mbatizaji, nikasema ndiye aliyekatwa kichwa kwa sababu ya Injili, akasema ndiye huyu. Basi akanikumbatia na kunishika mkono (Mathayo 14:1-11). Mtu wa tatu kunionyesha alikuwa ni Eliya Mtaabishaji wa Israel (1Wafalme 18:17-18) naye akanikumbatia na kunishika mkono, alinionyesha wengi sana akina Paulo, Petro na Yohana na wengineo. Batholomayo akasema, ‘Mpendwa, kawaambie wapendwa duniani, wakaze mwendo maana sekunde moja siyo muda mrefu’ (Filipi 3:12, 1Korintho 9:24-27), tukaondoka ile sehemu.
Wakanipeleka sehemu ambayo zinaandaliwa nguo za kuvaa watakatifu katika karamu ya Mwanakondoo, katika sehemu ile niliwakuta malaika wengi mno wakimsifi Mungu kwa shangwe. Katika sehemu hii pia kulikuwa na mashine nzuri zilizotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu mno, nguo nyingi sana ziliingia ndani ya mashine na kutolewa zikiwa zinang’aa sana, nikauliza mbona nguo zinatengenezwa nyingi sana, ni za nani? Maana watu wengi wanakataa wokovu. Akasema ‘Ninyi kaihubiri injili tu, anayetaka kuokoka na aokoke asiyetaka aache, kinachotakiwa ni kwamba anapokuja Mwana wa Adamu asiwepo wa kusema mimi sikusikia’
Basi tukaondoka ile sehemu. Ule mji ni sifa kila kinachofanyika, kilifanyika huku wakimsifu Mungu, si malaika wala si mwanadamu, si maua, si vinanda, maana vinanda vya kule vinapiga vyenyewe. Wakanipeleka katika ile sehemu ya awali iliyokuwa na viti vingi vyenye majina yaliyoandikwa kwa damu mbichi.
Tulipofika mara ya kwanza hakukuwa na mtu, lakini muda huu tulimkuta mtu mmoja aliyekuwa akifanya kazi kwa haraka sana, alikuwa amekazana sana kuliko Roboti. Nilimwuliza katika mji huu kuna watu wawili kama hawa? Tena kwa nini wamekazana sana hivi. Akasema huyu ni mtu mmoja kumbuka alipokuwa anaondoka duniani alisema, Ninakwenda kuwaandalia mahali ili alipo nanyi muwepo. (Yohana 14:1-6), akasema ‘huu mji ameuandaa mwenyewe hakuna mtu aliyemsaidia. Tena amekazana kwa sababu muda umefika wa kuchukua walio wake duniani’ (1Thesalonike 4:13-17). Wakaniondoa sehemu hii. Sehemu inayofuata ni sehemu muhimu sana, umesoma na kusikia zote za kwanza, sasa naomba utulie.
SURA YA 4
MANGOJEO NA JEHANAMU YA PILI:
Mmoja wa wale malaika akaniambia sasa tunakwenda kukuonyesha Jehanamu sehemu ya pili nikasema, Ah kuna sehemu nyingine tena? Akasema ‘Ndiyo, hii imezishwa ukari mara saba zaidi’ (Mithali 15:10).
Baada ya mazungumzo hayo, ndani yangu furaha ya uzima wa milele ikatoweka nikawaza iwapo sehemu ile nililia vile? Je hii itakuwaje? Nikawafuata katika sehemu hii ya mangojeo peke yake ilinitoa raha, kwa sababu ilikuwa ni kama mara saba zaidi ya ile ya kwanza. Watu wake walitoa sauti za uchungu mkubwa mara saba zaidi, watu niliowaona ni wale wote waliozijua siri za Mungu na kudharau, ni wale wote waliookoka na kuacha wokovu. (Ebrania 2:3, 6:4-6) Ni mchungaji na waalimu (Yakobo 3:1, Ezekieli 34:2-6) wanalia milele na milele bila kutoa chozi moja. Kabla hata ya kuonyeshwa nililia kwa uchungu sana na kuishiwa nguvu.
Akainuka mtu wa kwanza akasema, Bwana naomba umtume mtumishi wako aniletee tone la maji niuburudishe ulimi wangu. Mpendwa habu jiulize wewe upo duniani, je unaridhika na tone moja la maji? Basi sehemu ile tone la maji lina thamani sana wanalilia tone hilo usiku na mchana.
Malaika akawaambia mlipokuwa duniani mliichezea neema ya Mungu, sasa hivi ni sehemu ndogo sana ya mateso bado sehemu yenyewe. Yule mtu akajitupa na kuendelea kulia kwa uchungu mno nilimwangalia tena haikuinuka kabisa.
Nikaendelea kuwafuata wale watu huku nikilia na kutembea kwa taabu mno tukamkuta mtu wa pili akasema, Bwana utupe sekunde 10 tukaihubiri injili ulimwenguni ili waokoke. Yule Malaika akasema mlipokuwa duniani mlikuwa na muda mwingi sana wa kuihubiri injili lakini mliutumia kwa tama zenu sasa hii ni sehemu ndogo tu ya duniani nikalia kwa uchungu sana. Hakuinuka tena, mateso waliyonayo yanawafanya waombe sekunde 10 kuhubiri.
Mpendwa muda uliopoteza kwa mambo yasiyo ya maana utadaiwa, maana wewe ungehubiri injili Jehanamu ingekosa watu wa kwenda kwa sababu umetumia vizuri muda wako kuhubiri injili.
Mara nikasikia kigelegele cha kutisha mno nikauliza hivi, kuna mtu ametupwa motoni? Wakasema hapana. Tumesema jehanamu hii imezidishiwa ukali mara saba zaidi. Sasa kigelegele hicho ni cha moto kikishangilia kwa sababu muda wake umefika. Nikasikia mara nyingine tena, nikauliza vilevile nikaambiwa mbona wewe husikii, jehanamu hii imezidishwa mara saba zaidi. Wale watu wanasikia vigelegele vya kutisha lakini hawana la kufanya zaidi ya kusubiri mateso, tofauti na duniani ambapo mtu akipata shida kidogo anajiua, lakini sehemu hii haiepukiki. Tofauti nyingine tena ni kwamba duniani mtu anayo nafasi ya kutubu, lakini sehemu hii hakuna.
Ndani ya ule moto niliwaona FUNZA waliokonda sana, basi nikasikia sauti kutoka upande ule ikisema Bwana ‘watu uliosema utawaleta watakuja lini?’ Nikashituka na kuuliza je huku kuna mtu, funza hao waliongea lugha ya Kiswahili. Akawaambia wale funza subirini kidogo, hapo ndipo walipoonekana kuwa wamechokozwa. Hakukuwa na maelewano kabisa, walipiga kelele wakisema ‘chakula chetu’.
Akaniambia hao funza ulivyowaona wamekonda watakapomshika mwanadamu ipo kazi. Nililia sana hadi wale malaika wakaamua kuniondoa sehemu ile; akasema ‘sasa kawaambie watu wote duniani, usiongeze wala usipunguze’. Nikasema Bwana mimi duniani siendi wala hapa sikai nipeleke kwa wale wanaoimba. Basi akanigusa bega, nikashangaa natokea shambani saa kumi na mbili jioni na mama ndipo aliposhituka na kuja kuniona.
Sasa ndugu yangu, nimekueleza jinsi ilivyokuwa na sasa ni juu yako wewe kuchagua, sikuongeza wala sikupunguza (Mathayo 7:13-14, Kumbukumbu 3:19-20).
MIMI SITAONGEZA NA SASA NI KAZI KWAKO KUAMUA (Ufunuo 3:20)
MUNGU NA AKUBARIKI.